Nafasi ya Mungu katika maisha ya mwanadamu - Kanisani Kwanza

Nafasi ya Mungu katika maisha ya mwanadamu

Share This
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Nafasi ya kwanza ya mwanadamu maishani mwake inatakiwa kuwa ni kuutafuta ufalme wa MUNGU ambao uko pekee katika Wokovu wa KRISTO YESU.

Mathayo 6:33 "Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa."

Sio watu wengi huona jambo hili kuwa la muhimu kuliko yote wayafanyayo, lakini kwa mtu anayeuhitaji uzima wa milele anatakiwa kulifanya jambo hili kuwa la kwanza kwake.
Ni hatari sana kama mtu akiutumia vibaya muda wake wa kuishi duniani maana kama akiondoka bila YESU KRISTO atakosa uzima wa milele.


Mtu mmoja maarufu huko Marekani aliwahi kufuatwa na Mhubiri wa injili na kuambiwa kwamba anatakiwa kuokoka. Yule Mtu maarufu alimwambia yule mhubiri kwamba ''YESU wako uliyekuja naye hapa naomba uondoke naye maana mimi simhitaji'' Mhubiri yule alishangaa mno maneno ya yule mtu Maarufu lakini kumbe ile ilikuwa nafasi ya mwisho ya mtu yule maarufu kutubu na kumpokea YESU kama Mwokozi ili ahusike na uzima wa milele, lakini alipoichezea neema ya MUNGU kwa kukataa kumpokea YESU hakika siku chache baadae alifariki bila kuokolewa na YESU KRISTO,ni hatari sana.

Hata leo Neno hili limekuja kwako ndugu kwa sababu maalum, sababu hiyo ni kwamba unatakiwa kuokoka yaani kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kisha unaanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu.

Kama uliokoka na kurudi nyuma hakikisha unatubu na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Kama umeokoka na unaishi maisha matakatifu basi endelea hivyo ndugu huku ukiukomboa wakati.
Wakolosai 4:5 '' Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.''

Ndugu ambaye hujahusika na ufalme wa MUNGU, hakikisha leo unampokea YESU KRISTO kama Mwokoziu wako Binafsi.

Ndugu, usikubali kutafuta kwanza mengine kisha ufalme wa MUNGU baadaye.
Ndugu, usikubali kutafuta maisha kwanza huku ukipanga kuokoka baadae.
Ndugu, usikubali kutafuta kwanza mke/Mume harafu mambo ya Wokovu baadae.
Ndugu usikubali kutafuta pesa kwanza kisha ufalme wa MUNGU baadae.
Biblia inakutaka kutafuta kwanza ufalme wa MUNGU na haki yake.
Haki ya ufalme wa MUNGU ni utakatifu katika KRISTO YESU.
1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''

Wengi walitafuta maisha kwanza na hawakuyapata na huku ufalme wa MUNGU pia wameukosa.
Wengi walitafuta dunia kwanza na hawakuimaliza huku ufalme wa MUNGU wameukosa, wakiambulia magonjwa na majeraha tu.
Wengi walitafuta mambo yao kwanza lakini hata hayo hawakuyapata.
Ndugu mpendwa nakuomba ifuate Biblia ndio utafanikiwa.
Na Biblia inakushauri kwamba utafute kwanza ufalme wa MUNGU na hayo mengine utazidishiwa na MUNGU.
Ndugu utafute ufalme wa MUNGU kwanza.
Kwa umuhimu mkubwa sana Biblia pia inautaja ufalme wa MUNGU kwa jina la Ufalme wa Mbinguni, kama sehemu ya kukupa msisitizo.
Mathayo 3:2 ''Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.''

Kuna watu wana juhudi sana katika kutafuta pesa lakini kwa sababu hawana ulinzi wa MUNGU ndio maana hujikuta wakinufaisha wengine wanaotumia nguvu za Giza.
Sio kwamba usifanye kazi Kabisa, hapana, Bali Fanya kazi ukiwa ndani ya ufalme wa MUNGU.
Mpate Mwenzi ukiwa ndani ya ufalme wa MUNGU na yeye awe yuko katika ufalme wa MUNGU ndipo itakuwa kustawi kwako na kufanikiwa kwako.
Itafute mbingu kwanza.
Mtafute MUNGU kwanza .
Mtii YESU KRISTO Mfalme wa ufalme wa MUNGU.
Na kumtii YESU ni kutii maagizo yake yote anayoagiza katika Biblia takatifu. Yeye Bwana YESU anasema " Yeye anichukiaye mimi humchukia na Baba yangu.- Yohana 15:23
Pia anakushauri kwamba litii Neno lake.
Yohana 14:15 "Mkinipenda, mtazishika amri zangu."
Ndugu yangu utafute kwanza ufalme wa MUNGU.
Neno hili ni lako maana ni ufunuo kwa ajili yako.
Ana heri mtu anayeupokea ufalme wa MUNGU na mtu huyo amejitenga na kila njia zinazoweza kumtoa katika kweli ya MUNGU ambayo ni KRISTO.
Biblia inasema ''Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.-Zaburi 1:1-3''
Huu ni wakati wa kuutafuta ufalme wa MUNGU.
Ndugu usikubali ufalme wa MUNGU ukupite kwa sababu ya ukaidi wako.
Hata kwa watu waliookoka ni muhimu sana kufanya kazi ya kuhubiriufalme wa MUNGU kwa kila mtu iwe ni katika jamii, ukoo au marafiki.
Mteule wa MUNGU uliyeokolewa na Bwana YESU unayo nafasi kubwa katika ukoo wako na familia yako.
Nafasi hiyo ni MUNGU amekupa.
Itumie nafasi yako vyema.
Itumie nafasi yako kuwafundisha ukoo wako na familia yako kuhusu ufalme wa MUNGU.
Usipowafundisha ujue wanaweza wakakosa uzima wa milele.
Askari magereza mmoja kwenye Biblia alipopata Neema ya kumpokea YESU alihakikisha na familia yake wanaokoka kama yeye.
Matendo 16:30-34 " kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana YESU, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.
Wakamwambia neno la BWANA, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake. Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo.
Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini MUNGU."
Je wewe baada ya kuokoka unachukua juhudi gani kwa ajili ya ndugu zako kuokolewa na Bwana YESU?
Ndugu itumie nafasi yako vyema kwa ajili ya ufalme wa MUNGU.
Unajisikiaje ndugu, wewe uende mbinguni harafu ndugu zako wote waende jehanamu?
Baba/Mama uende mbinguni lakini watoto wako na mwenzi wako waende jehanamu!?
Ndugu itumie vyema nafasi yako aliyokupa MUNGU kwa kuwafanya ndugu zako waokoke.
Wewe ambaye hujaokoka nakuomba hakikisha unaokoka.
'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22 ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

No comments:

Post a Comment