Wema ni akiba - Kanisani Kwanza

Wema ni akiba

Share This
Kuna mwanamke tajiri alikuwa akiendesha gari lake, katikati ya njia gari likaharibika, akateremka na kuomba lifti, lakini magari yalikuwa yanampita bila kusimama. Alisimama muda mrefu barabarani bila mtu kumsaidia, Mvua ikaanza kunyesha, akaanza kuogopa isije kufika usiku naye yuko barabarani, baada ya muda mfupi akaona gari bovu linakuja akalisimamisha, lakini alikuwa na wasiwasi kuhusu dereva asije kuwa mtu wa hovyo.

Mwisho akaamua kulisimamisha lile gari na yule dereva akasimama, mwanamke akapanda wakaondoka. Akamuona yule mwanaume anaonyesha ni mtu masikini mwenye shida, yule mwanamke akamuona yule mwanaume ni mtu wa heshima, akajilaumu ndani ya nafsi yake kwa kumdhania vibaya, Mwanamke akamuuliza yule mwanaume jina lako nani? Na unafanya kazi gani? Yule mwanaume akamjibu 'Mimi naitwa Adam na kazi yangu ni dereva.

Baada ya muda wakafika Mjini, yule mwanamke akamwambia 'naomba usimamishe gari Mimi nitashuka hapa,' Yule mwanaume akasimamisha gari, Mwanamke akamuuliza kuhusu nauli yake kiasi gani? Yule mwanaume akamjibu: Nimekusaidia sitaki kitu halafu akaondoka zake. Yule mwanamke akashangaa sana jinsi yule mwanaume alivyo na utu.



Mwanamke akaona Coffee Shop akaingia, akamuita Mhudumu, wakati Mhudumu anakuja akawa anamuangalia anavyotembea, alikuwa amechoka sana kwa Ujauzito.

Yule mwanamke akamuuliza kwa nini unajihangaisha? Yule Mhudumu akamjibu najihangaisha ili nipate pesa ya kujiandaa, maana karibuni nitajifungua. Halafu akaenda kumletea kahawa aliyoagiza. Yule Mwanamke akanywa kahawa yake mpaka akamaliza. Halafu akamuita Mhudumu ili amlipe, Mhudumu akachukua pesa akaenda mpaka kwenye meza ya malipo, halafu akachukua chenchi iliyo baki ili amrudishie yule mwanamke.


Chenji ilikuwa ni pesa nyingi ambayo yule mwanamke angeweza kunywa vikombe zaidi ya 10. Yule mhudumu alipofika ktk meza ya yule mwanamke hakumuona, akatizama kulia na kushoto mwanamke hayupo,alishaondoka, akaona kwenye meza kikaratasi kimeandikwa, chenchi iliyobaki ni zawadi yako, alifurahi sana mpaka machozi yalimtoka, alivyokuwa anachukua ile karatasi akaigeuza upande wa pili akaona imeandikwa.

"Na hapo chini ya meza kuna zawadi ya mwanao" alitizama chini ya meza akaona kuna pesa nyingi, pesa kama za mshahara wake wa miezi 6, alitamani apige kelele kwa furaha, aliomba ruhusa kazini mapema ili arudi kwake.

Aliporudi akawa anapiga kelele anamtafuta mumewe, Mume kusikia zile kelele alishangaa sio kawaida yake kurudi muda huo, alidhani kuwa labda mkewe anaumwa na uchungu, lakini sauti ya kelele ilikuwa ni sauti ya furaha, mke akamuita Mumewe Adam uko wapi mume wangu? Mke akaendelea kusema Mungu ametuteremshia neema yake nimepata neema kwa mwanamke mwenye kheri, shida zetu zimekwisha.


Je, mnamjua Adam mwenyewe ni nani? Adam ni yule aliyempa lifti yule mwanamke na ndio mumewe.
Ukifanya WEMA unajifanyia Mwenyewe utakurudia na ukifanya UBAYA unajifanyia Mwenyewe.

No comments:

Post a Comment