Je uongo una nafasi gani katika mahusiano? - Kanisani Kwanza

Je uongo una nafasi gani katika mahusiano?

Share This
Mithali 20:17 "Chakula cha uongo ni kitamu kwa mtu; Lakini halafu kinywa chake kitajaa changarawe"
Mithali hii inamaanisha kuwa, mara nyingi mtu anaweza kunufaika kwa maneno ya udanganyifu lakini mwisho wake, aliyedanganya na aliyedanganywa wanadhurika, matokeo ya uongo, udanganyifu au hila ni madhara sawa na mtu anayejikuta anatafuna changarawe badala ya chakula.
Vijana wengi na hata wazee, wakike na wakiume, wamejikuta wanatafuna changarawe au kokoto, badala ya UTAMU wa mapenzi walioanza nao, wengi wamejeruhiwa na wenzi wao waliojidai wanawapenda, kumbe wana mapenzi ya hila na udanganyifu.

Japo kuna wavulana wanao TOSWA na mabinti, tena wengine baada ya kuwagharamia hata masomo, lakini asilimia kubwa ya majeraha ni mabinti, wavulana wengi ni wadanganyifu, japo wanaanza kwa mahaba mubashara, wanaishia kujeruhi na kuumiza.

Neno la leo, linawaonya vijana wa kiume na mabinti, UONGO una madhara kwa wote wawili, japo wavulana wanajiona wana uhuru wa Kuharibu na kutafuta wengine, LAANA ya udanganyifu inawafuata hadi kwenye ndoa zao, vivyo hivyo kwa wasichana wadanganyifu.

Vijana; muombeni Mungu, msidanganye wala kudanganywa. Mabinti usikubali mahusiano ya ku "PASS TIME", muda ukipita haurudi na huku sifa za Ubinti zikizidi kuyoyoma. Usikubali kuwa chombo cha KITULIZO, ndani ya shimo la udanganyifu ... UTAUMIA.

Kumbuka; kisasi ni cha Mungu kwa kila aliyemuumiza mwenzie, na yeyote aliyetendwa, Bwana atamtegemeza.

MUNGU AWAPATIE SIKU NJEMA YENYE MIANZO MIPYA

Mwandishi; Mchungaji Eliezer Mwangosi- +255 767 210 299

No comments:

Post a Comment