MBINU ZA KUKUSAIDIA KUOMBA VIZURI KWA MUDA MREFU
1. CHAGUA MAHALI PAZURI PA UTULIVU. *Mk 1:35
ili uweze kuomba kwa utulivu na kwa umakini, chagua au tafuta mahali pazuri
patakapokupa utulivu katika kuomba (concentration in prayer). Ndio maana Mungu
alipenda kuongea na Musa juu ya mlima. (Kut 24:12-18). Hata Yesu alizoea kwenda
kuombea mlimani, mahali palipo mbali na vurugu za watu, alipenda kwenda mlimani.
2. CHAGUA MUDA MZURI. *Mhu 3:1,7
Ili uweze kuomba kwa umakini mzuri, chagua muda mzuri ambao akili yako ma mwili
wako viko fresh. Usilazimishe kuomba hata kama akili yako
au mwili wako umechoka sana. Kila jambo lina wakati wake. Kama umechoka
sana, huo si muda wa kuomba, bali wa kupumzika. Usilazimishe ratiba. ni
bora upumzike ili baadaye uweze kuomba vizuri baadaye. Usije ukajikuta
unamkemea Yesu badala shetani. Penda kuomba wakati una nguvu ya akili na
mwili, ili uwe makini kuongea na Mungu kwa akili timamu. Ndio maana
Yesu alipenda kuamka alfajiri sana kwenda kuomba mlimani. (Mk 1:35, Luka
4:42)
3. OMBA KATIKA ROHO (NENA KWA LUGHA). *Efe 6:18, Rum 8:26-27
Mbinu nyingine nzuri ya kuomba kwa muda mrefu na kwa
ufanisi, ni kuomba kwa Roho; yaani kuomba kwa kunena kwa lugha.
Tunapoomba kwa akili za kibinadamu, Mungu anasikia pia, lakini maombi
yako yanakuwa na mipaka / limited kwasababu akili ya mtu haijui kila
kitu. Bali Roho wa Mungu anajua kila kitu. Naye hutupa kipawa cha kuomba
kwa lugha ya mbinguni iliyo bora zaidi. (Yuda 1:20, Mk 16:17, 1Kor
14:1-4, 15-16,7)
4. OMBA KWA KUFUNGA WAKATI MWINGINE. *Math 6:16-18
Kufunga kula kunasaidia kudhoofisha mwili, ili roho iwe
makini zaidi kuongea na Mungu kwa kina zaidi. Mwili huu siku zote
haupendi kufanya mambo ya Mungu. Na mwili ukiwa umeshiba, unakuwa na
uchovu na uzito wa kufanya mambo ya kiroho. Mbinu mojawapo ya
kuudhibiti, ni kuunyima/kuupunguzia posho yake ya chakula. Mwili
ukidhoofika kiasi, roho yako inapata nguvu na upenyo mzuri zaidi (Zab
35:13). Mashujaa wote wa imani walifunga na kuomba. Ndio maana Yesu
anasema ‘mfungapo’ akimaanisha ratiba ya kufunga, ipo. Inasaidia.
5. OMBA NA RAFIKI (PRAYER PARTNER). *Mhu 4:9-10
Neno la Mungu linasema, ni heri wawili kuliko mmoja. Kuna
faida ya kuomba pamoja na rafiki yako. Kwanza, mnapokuwa wawili au
watatu, inaleta hamasa na ari ya kuomba zaidi. Si rahisi kujisikia mvivu
unapokuwa na waombaji wenzako. Pili; nguvu ya kiroho inaongezeka. Neno
linasema, mwombaji mmoja anafukuza adui elfu moja, bali wakiwa wawili,
wanafukuza (sio elfu mbili) bali elfu kumi! Shangaa! (Kumb 32:20) Hiyo
ni kanuni ya mbinguni/kanuni ya Ki-Mungu. Kadri mnavyoongezeka, nguvu ya
Mungu huongezeka.
Kwahiyo, wakati mwingine, omba na rafiki yako,
unayemwamini, unayeweza kumshirikisha mambo yako ya binafsi. Mashujaa
wengi wa imani, walikuwa na marafiki wa kiroho. (Prayer Partners). Kwa
Mfano:-Math 17:1-9
Musa – alikuwa na Joshua, Haruni na Huri
Eliya – alikuwa na Elisha
Daniel – alikuwa na Shadrack, Meshack na Abednego.
Yesu – alikuwa na Petro, Yakobo na Yohana.
Paul – alikuwa na Barnaba, Timotheo na Tito.
Wewe Je? Uko na nani katika urafiki wa kiroho?
Kama huna rafiki wa karibu wa kuomba naye, usikurupuke
kujichaglia. Tulia umwombe Mungu akupe mtu atakayekuwa wa msaada kwako.
Mtu mtakayefungamanishwa naye katika roho, hata kama mmetengana
kijiografia, lakini katika roho, mko na umoja mzuri wa imani. (Math
18:18-19)
6. OMBA KATIKA MKAO UNAOKUPA UHURU NA NGUVU ZAIDI.
Katika kuomba kwa muda mrefu, mkao uliouzoea utakusaidia
kwenda mwendo mrefu. Yakupasa kujua nguvu yako na udhaifu wako (strong
point and weak point). Wakati wa kuomba, epuka mikao inayokuchosha
haraka na tumia mikao inayokua nguvu zaidi. Kwa Mfano:- Ukiwa umechoka,
usipende kuomba kwa kupiga magoti au kwa kuegemea kitandani. Ni bora
uombe ukiwa umesimama au unatembea tembea, ili kuepuka usingizi na
uchovu. Waombaji hodari wanaujua mikao inayowasaidia kuomba maombi
marefu. Wengine hawana mikao maalum, bali wakiwa katika maombi, huwa
wanabadilisha-badilisha mikao ili wasichoke. Hiyo ni mbinu nzuri pia.
Mifano ya Mashujaa wa imani;
Ibrahim – aliomba kwa kusimama (Mwa 18:22)
Daniel – aliomba kwa kupiga magoti (Dan 6:10)
Paul – aliomba kwa kupiga magoti (Efe 3:14)
Yesu – aliomba kwa kulala chini (Math 26:38-39)
Eliya – aliomba kwa kukaa chini na
kuweka kichwa kati ya miguu (1Fal 18:42)
Mimi – huwa napenda kuomba kwa kutembea tembea
Naweza kumaliza kilomita nyingi chumbani kwangu
Nikitembea huku nikiomba.
Wewe Je? Unaujua mkao wa nguvu? Kama hujui, Tafuta kujua.
7. OMBA NA MUZIKI LAINI KWA KUMWABUDU MUNGU.
Muziki wa kiroho, na wataratibu, unaweza kukutengenezea
mazingira mazuri sana ya kuomba kwa muda mrefu. Muziki wa kuabudu,
unavuta uwepo wa Mungu kwa namna ya pekee. Neno linasema, waimbaji na
wanamuziki walipoimba na muziki ukapigwa, nao wakawa kama mtu mmoja,
utukufu wa Mungu ukashuka na kulijaza lile hekalu hata makuhani
hawakuweza tena kuhudumu (2Nyak 5:12-14). Kule mbinguni, kila malaika wa
sifa, ana kinubi (zeze/gitaa). Elisha hakutoa unabii, mpaka mpiga
kinubi alipopiga kwa ustadi, ndipo mkono wa Bwana (Roho wa Mungu)
alipokija juu yake, naye akatabiri.
Najaribu kukuonyesha, kuna connection kati ya muziki wa
kiroho na utukufu wa Mungu. Kwahiyo, ukiweza kuomba huku umeweka kanda
au CD ya nyimbo za kiroho za taratibu, utapata (experience) hamasa ya
kiroho (motivation) na utasikia una nguvu ya kuomba kwa muda mrefu. Kama
unaweza, tengeneza kanda au CD maalum yenye nyimbo nzuri unazozipenda
wewe, ili uwe unaipiga wakati wa maombi. Utajikuta unaweza kuomba kwa
muda mrefu na kwa bubujiko zuri zaidi
MWISHO...
Mwalimu Mgisa Mtebe
MWISHO...
Mwalimu Mgisa Mtebe
No comments:
Post a Comment