Msiipende Dunia - Kanisani Kwanza

Msiipende Dunia

Share This
1 Yohana 2:15-17
“MSIIPENDE DUNIA, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, TAMAA ya MWILI, na TAMAA ya MACHO, na KIBURI CHA UZIMA, havitokani na Baba, bali vyatokana na DUNIA. Na dunia inapita, pamoja na TAMAA ZAKE, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.”
‭‭ 1). MWILI NI NINI?
Tunapozungumzia juu ya MWILI kwa kiyunani ni "SARX". Ni nyumba ya roho na nafsi. Nafsi na Roho zinakaa ndani ya nyumba inayoitwa MWILI. Mwili ulifanyizwa na Mungu kutokana na udongo au mavumbi ya ardhi. Kwahiyo asili ya mwili ni udongo. Asili yake ni ardhini. Roho na Nafsi zimetoka kwa Mungu lakini mwili ulifanyizwa kwa mali ghafi ya udongo.

Mwanzo 2:7
“BWANA Mungu akamfanya mtu kwa MAVUMBI YA ARDHI, akampulizia puani PUMZI YA UHAI; mtu akawa NAFSI HAI.”
Mwanadamu amegawanyika katika sehemu kuu tatu nazo ni:-
i). Mavumbi ya Ardhi - MWILI
ii). Pumzi ya Uhai - Roho
iii). Nafsi Hai - Nafsi
1 Wathesalonike 5:23
“Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.”
‭‭
Kifupi MWILI ni jumba la ROHO.
Mtu anapokufa mwili huirudia ardhi bali roho humrudia Mungu aliyeitoa kwa ajili ya maisha umilele (iwe ni Mbinguni au Motoni)
Mwanzo 3:19
“kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe MAVUMBINI UTARUDI.”
Mhubiri 12:7
“Nayo MAVUMBI KUIRUDIA NCHI kama yalivyokuwa, Nayo ROHO KUMRUDIA MUNGU aliyeitoa.”

Utakumbuka kwa habari ya maskini Lazaro na Tajiri katika kitabu cha Luka 16:19-31, Maskini Lazaro alienda Mbinguni bali Tajiri alienda kuzimu sehemu yenye mateso. Kwahiyo kuna maisha baada ya kifo.
‭‭2). TAMAA YA MWILI
Biblia inapozungumzia tamaa ya mwili inazungumzia tamaa mbaya inayosababishwa na mwili. Mwili hutuvuta kutenda matendo ya mwili. Kwa kuwa mwili asili yake ni udongo muda mrefu hutuvuta kufanya mambo ya mwilini. Mwili wakati wote hufanya mashindano na roho zetu ndiyo maana wakati mwingine roho zetu zinahitaji kuwasiliana na Baba yetu wa Mbinguni aliye Roho, mwili "husema nimechoka ngoja nilale kidogo".
Wakolosai 2:23
“Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia TAMAA ZA MWILI.”
1 Petro 2:11
“Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni TAMAA ZA MWILI zipiganazo na roho.”
‭‭ Mtu yeyote anayeyafuata matendo ya mwili hawezi kumpendeza Mungu. Maana kile ambacho mwili hutaka na ukafuata hicho kamwe hauwezi kumpendeza Mungu. Kufuata Tamaa za mwili ni dhambi itakayotupeleka motoni.

Warumi 8:5-8
“Kwa maana wale WAUFUATAO MWILI HUYAFIKIRI MAMBO YA MWILI; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa NIA YA MWILI NI MAUTI; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni UADUI JUU YA MUNGU, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili HAWAWEZI KUMPENDEZA MUNGU.”
Nia ya mwili ni Uadui juu ya Mungu. Ikiwa tunataka kumpendeza Mungu ni lazima tufuate matakwa ya roho. Siyo kila kitu mwili inachokitamani ukipe, HAPANA. Mwili lazima ukataliwe matakwa yake ambayo yanatupelekea kumtenda Mungu dhambi. Hapa sizungumzi juu ya mwili kutamani kuoga, au kutamani Tendo la Ndoa kwa yule aliyeko kwenye Ndoa, kutamani kuvaa nguo nzuri, kutamani kusoma n.k. Huko ni kutamani kuzuri na wala si dhambi.
‭‭
3). MATENDO YA MWILI
Baada ya anguko la Mwanadamu katika dhambi kila anayezaliwa na mwanadamu kupitia mwanaume na mwanamke kukutana kimwili anazaliwa akiwa amechukua asili ya MWILI WA DHAMBI. Mwili huu wa dhambi ambao mwanadamu anao una Matendo yake. Matendo ya mwili wa dhambi ni kama yafuatavyo:-
Wagalatia 5:19-21
“Basi MATENDO YA MWILI ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu."
‭‭
Warumi 1:24, 26-27
“Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika TAMAA ZA MIOYO YAO, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima MIILI YAO. Hivyo Mungu aliwaacha wafuate TAMAA ZAO ZA AIBU, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, WAKAWAKIANA TAMAA, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.”
SEMA MANENO HAYA:-
Mungu Baba ninakuja mbele zako. Nimetambua Mimi ni mwenye dhambi kwa Matendo ya mwili ninayotenda. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote kuanzia sasa. Nifunike kwa wema na rehema zako. Asante Baba kwa kunisamehe na kuniokoa katika jina la Yesu.
Amen!!!!!!!

Bishop Emmanuel Mbagwile (+255 715 136868)

No comments:

Post a Comment