Hatua na vipengele muhimu katika kufanya Maombi-Sehemu 1 [Mwl. Mgisa Mtebe] - Kanisani Kwanza

Hatua na vipengele muhimu katika kufanya Maombi-Sehemu 1 [Mwl. Mgisa Mtebe]

Share This
Hatua na vipengele muhimu katika kuomba
 1. MKARIBISHE ROHO MTAKATIFU. *Rum 8:26-27 *Yoh 14:16-17
Yesu alisema Roho Mtakatifu ni msaidizi wetu. Atatusaidia na kutufundisha yote, kwa maana pasipo yeye, sisi hatuwezi neno lolote. Na sisi peke yetu hatujui kuomba ipasavyo, bali yeye (Roho) ajua kutuombea kwa Mungu kama vile Mungu apendavyo. Hivyo kabla ya kuanza maombi au kusoma neno au ibada au safari au mitihani au kikao n.k. jifunze kujikabidhi kwa Roho Mtakatifu, uombe msaada wake, akupe ufanisi/ubora katika yote yakupasayo kufanya.
Tambua Utu wake, Uungu na Uweza wake.
Jikabidhi katika Nguvu ya Uongozi wake.
Tii kila Uongozi anaokupa.

2. FANYA TOBA NA UTAKASO. *Isa 59:1-2, Yoh 9:31, 1Yoh 1:8-9,7
Sikio la Bwana si zito kusikia wala mkono wake si mfupi kushindwa kututendea mambo tumwombayo, bali maovu yetu ndiyo yanatufarakanisha na Mungu wetu. Mungu hawasikii wenye dhambi. Hivyo chukua muda wa kutafakari na kuungama dhambi zako mbele za Mungu na kuzitubu kwa kumaanisha kuziacha. Mungu ni mwaminifu kutusamehe na kututakasa na uchafu wote. (Isa 1:18). Lakini, kabla hujafanya toba yako binfsi;
(i) – Kwanza, samehe wote waliokukosea, hata kama hawajaja
kukuomba msamaha. Usipowasamehe waliokukosea, na Mungu
hataweza kukusamehe wewe. (Math 6:12,14-15)
(ii) – Ndipo nawe ufanye toba yako binafsi. Na Mungu atakusamehe kabisa.
Hata kama ni nyekundu sana, zitakuwa nyeupe sana. (Isa 1:18, Isa 43:25)
3. MSIFU, MUABUDU NA KUMSHUKURU MUNGU. *Zab 147 na Zab 148
Msifu Bwana kwa Matendo yake makuu, mwabudu Bwana kwa uzuri wake na kwa sifa zake. Mwadhimishe Mungu kwa Tabia zake, wema wake, fadhili zake na baraka zake mbalimbali anazotutendea. Sifa yako ikifika vizuri mbele za Mungu, ndipo atakuwa tayari kukupa haja za moyo wako. Haja zetu zimefichwa nyuma ya mgomgo wa sifa. Ndio maana Neno linasema;
‘Nawe utajifurahisha kwa Bwana (kwa kumsifu, kumwabudu na kumshukuru), naye atakupa
haja za moyo wako’ (Zab37:4).
Yesu anatuonyesha mfano; angalia sentensi yake ya kwanza katika kuomba kwake imekuwa “Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe.” (Math 6:9). Anaanza maombi kwa kumsifu Mungu. Msifu Mungu kwa kuimba na kwa kunena/kusema/kuelezea. Mungu anataka kusifiwa na kutukuzwa. Ukifanya sifa nzuri, ya kuufurahisha moyo wake, atakupa hata na vile ambavyo hukutegemea/hukuomba.
4. MWELEZE MUNGU MAHITAJI NA HOJA ZAKO. *Wafilipi 4:6-7,19 Isa 43:26
Mweleze Mungu zile hoja zilizokusukumwa kwenda kumwomba. Nenda mbele za Mungu kama ‘kuhani’ (1Pet 2:9). Kwa unyenyekevu na heshima. Lakini kabla ya kumweleza mahitaji yako binafsi;
(i) Kwanza fanya ‘maombezi’ – ombea watu wengine; (1Tim 2:1-4)
Viongozi mbalimbali na wenye mamlaka, watumishi wa Mungu, marafiki zako, wenye shida, ndugu zako, nchi yako, shule yako, shirika lenu, ofisi yenu, chama chenu, n.k. Usianze kujiombea mwenyewe tuu, zoea kuwatanguliza wengine.
(ii) Kisha fanya ‘maombi yako’– ombea haja za moyo wako. (Math 7:7-11)
Mweleze Mungu haja zako. Ongea na Mungu kwa uwazi na ukweli. Japo anazijua haja zetu, lakini ameagiza kuwa tumwombe ndipo atafanya. ‘aombaye hupokea’ yaani; asiyeomba, hapati. Mungu anasema tumpelekee hoja zenye nguvu (Isa 41:21). Omba vitu vizuri na mambo makubwa ili upewe (pray for good things and big things)

5. FANYA MAOMBI YA VITA VYA ROHONI. *Efe 6:10-13 *2Kor 10:3-5
Baada ya kumwendea Mungu na kumweleza mahitaji yako, sasa simama kama ‘mfalme’, kwasababu wewe ni ‘mfalme’ (Ufu 5:8), tumia mamlaka yako ya kifalme, ongea na hali/hitaji ulilokuwa unaliombea, na kwa mamlaka, amuru iwe kama vile ulivyoomba/unavyotamani. Ndio maana Bwana Yesu alipokabidhiwa mamlaka yote na Mungu, naye akatukabidhi sisi (kanisa lake) “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule adui. Wala hakuna kitakachowadhuru” (Luk 10:19, Yer 1:10, Yak 4:7). Tuma neno lenye mamlaka katika hali/jambo ulilokuwa unaliombea, Amuru iwe vile ulivyokuwa unamwomba Mungu iwe. Kemea kila roho ya shetani inayoweza kuwa inasababisha tatizo katika swala lako.
6. OMBEA ULINZI JUU YA ULIYOYAOMBEA. *Math 6:13a
Baada ya kupiga vita vya kiroho, weka ulinzi katika yale uliyoyaombea, ili shetani na mapepo yake wasiweze kuirudia hali/jambo/mtu yule uliyemkomboa kwa maombi ya vita. Yesu alisema shetani akifukuzwa mahali, haendi mbali, anasubiri kuona kama atapata upenyo wa kuparudia mahali pale alipokuwa kwanza. (Math 12:43-45). Kwahiyo, usipoweka ulinzi, kuna uwezekano wa adui kurudi na kuliharibu zaidi lile jambo uliloliombea na kulipata.
Kumbuka, unapoomba vizuri, unapokea papo hapo (katika ulimwengu wa roho), lakini udhihirisho wake katika ulimwengu wa mwili, unaweza kuchukua muda fulani. Hivyo katika muda huo wa kusubiri, shetani anaweza akapita na kuzuia au kuharibu kile unachokisubiri kidhihirike katika ulimwengu wa mwili. Ndio maana Yesu alitufundisha kuombea ulinzi, “tuokoe na yule mwovu” (Math 6:13a). Weka ulinzi juu ya mambo yako yote. Jengea wigo wa moto wa mbinguni (2Fal 6:16-17), Yafunike kwa damu ya Yesu na agiza malaika walinzi walinde mambo yako masaa yote. Omba hivyo kila siku. (Zab 34:7, Zab 91:9-11, Ebr 1:13-14)
7. MSIFU, MWABUDU NA KUMSHUKURU MUNGU. *Math 6:13b
Yesu alianza maombi kwa kumsifu Mungu na kumtukuza. Na akamaliza maombi yake kwa kumtukuza Mungu tena. Akasema “kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu ni zako, sasa na hata milele” akamaliza. Kwahiyo nawe kwa kumaliza maombi yako, msifu na kumshukuru Mungu tena, kwa ukuu wake, uaminifu wake, na ahadi zake juu yetu. Ndipo ufunge maombi yako.
MUHIMU: TUMIA MAANDIKO KATIKA KUOMBA *Kol 3:16
-Katika kuomba kwako, mara zote tumia maandiko kumkumbusha Mungu ahadi zake .(Isa 43:26). Mungu analiangalia neno lake ili alitimize. Sababu pekee itakayomfanya Mungu akupe alichoomba, ni ili kulitimiza neno lake. Hivyo, baada ya kumweleza unachohitaji (kwa ajili yako au kwa ajili ya mtu unayemwombea) mpe Mungu andiko/neno lake linalokupa wewe uhalali wa kuomba hicho kitu mbele zake na kupewa.
-Hata unapompinga na kumkemea shetani, baada ya kutoa amri yako dhidi yake, shetani atasubiri kusikia andiko/neno linalomnyima yeye uhalali wa kushika alichoshika. Ndio maana Yesu alimshinda shetani kwa neno la Mungu. Alisema “imeandikwa” na shetani akashindwa. “Nao wakmshinda (shetani) kwa damu ya Yesu na kwa Neno” (Ufu 12:11)
Katika sehemu ya pili nitakuletea mbinu zinazokusaidia kuomba kwa muda mrefu
Mwandishi; Mwalimu Mgisa Mtebe- +255 713 497 654
Imekaririwa na Barnabas Gwakisa

No comments:

Post a Comment