Biblia
imeandika mengi yanayotuonya kujihadhari na kujiweka tayari kukabiliana
na matukio ya kinabii yaliyotabiriwa kutokea katika kipindi cha siku za
mwisho ambacho sisi ndio kizazi husika.
Jumapili iliyopita
nilitimiza ahadi yangu kwa kuichambua “Kalenda ya kinabii” ambayo ni
baadhi ya matukio ya kinabii yanayotarajiwa kutimia wakati huu, kwa
maana katika kizazi hiki kilichopo hivi
sasa. Ninasema kizazi hiki kwa sababu kalenda ya siku za mwisho ilianza
rasmi tangu siku ya Pentekoste (MDO. 2:14-18) mpaka Yesu atakapolinyakua
kanisa lake kutoka duniani. (YH.14:2-3)
Mwishoni mwa mwaka
jana tumeshuhudia suala la mji wa Yerusalemu lilivyochukua nafasi kubwa
katika Umoja wa Mataifa ambapo mataifa yamegawanyika kuhusu hali ya
mgogoro wa Mashariki ya Kati baina ya Israeli na Palestina kuhusu mji wa
Yerusalemu. Macho ya jumuiya ya kimataifa hivi sasa yameelekezwa kwa
Israeli kuliko ilivyokuwa kabla huko nyuma.
Haya yanahusiana
kwa vipi na unabii wa Yesu Kristo kuhusu Israeli na Yerusalemu? Hii ni
mojawapo ya ishara ya tishio kuibuka vita kali Mashariki ya Kati ambayo
itahusisha mataifa makubwa ya Ulaya pamoja na mataifa ya kiarabu
yanayoizunguka Israeli.
Baadhi ya mambo niliyochambua jumapili iliyopita ni kama ifuatavyo:
UNABII KUHUSU “KUNYAKULIWA KWA KANISA”
Unabii wa siku za mwisho unatuonya kuhusu dalili za matukio ambayo
yanatarajiwa kutokea wakati wowote kuanzia hivi sasa ambapo baadhi yake
ni pamoja na; “unyakuo wa kanisa na kipindi cha dhiki kuu kilichotabiwa
na nabii Danieli pamoja Yesu Kristo mwenyewe.
Kwa habari ya
unabii kuhusu unyakuo wa kanisa tunasoma ahadi ya Yesu Kristo mwenyewe
alipotoa ahadi maalum ya kwenda kuandaa mahali na kisha kurudi tena
kuwachukua wanafunzi wake:
“Nyumbani mwa Baba yangu mna makao
mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi
mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe
kwangu; ili nilipo mimi nanyi mwepo.” (YH.14:2-3)
UNABII KUHUSU “KIPINDI CHA DHIKI KUU DUNIANI”
Unabii unapotaja habari ya kipindi cha dhiki kuu, unalenga “dhiki
tofauti na dhiki nyingine zote ambazo zimekuwepo duniani katika vizazi
vyote vilivyokwisha kutangulia." Kwa maneno ya Yesu Kristo mwenyewe
tunasoma ya kwamba:
“Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki
kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa,
wala haitakuwapo kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka
mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.”
(MT.24:21-22)
Soma vizuri maandiko kama “dhiki kubwa” ambayo
“Haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa” na wala
“haitakuwepo kamwe”! Haya ni maneno ya Yesu mwenyewe wala si manabii
wengine.
Kwanini ni dhiki tofauti kuliko dhiki nyingine zote?
Kwa sababu itakuwa imebeba ghadhabu ya Mungu dhidi ya uasi unaotarajiwa
kushika hatamu wakati wa kipindi cha dhiki kuu.
JE! UNYAKUO UTAFANYIKA LINI: KABLA AU BAADA YA DHIKI KUU?
Kumekuwepo malumbano sugu baina ya kambi za nadharia kuhusu kanisa
kunyakuliwa kabla au baada ya dhiki kuu. Kambi moja inaaamini na
kutafsiri kwamba kanisa la Kristo litakuwepo kwenye dhiki kuu. Kambi ya
pili inakanusha mtazamo huu na kufundisha kwamba kanisa litanyakuliwa
kabla ya kipindi cha dhiki kuu kuanza.
Uchunguzi wangu katika
maandiko na tafsiri yake kuhusu unyakuo na kipindi cha dhiki kuu,
nimebaini ya kwamba, fundisho la "kanisa kunyakuliwa kabla ya dhiki kuu"
lina ushahidi wenye ushawishi mkubwa kimaandiko. Nitaeelezea baadhi ya
ushahidi huo kama ifuatavyo:
UNABII WA DHIKI KUU UNAIHUSU ISRAELI NA SIO KANISA
Sababu kubwa ya Kambi ya nadharia inayofundisha kwamba kanisa
litakuwepo wakati wa dhiki kuu ni tafsiri isiyo sahihi ya kutokutambua
uwepo wa taifa la Israeli katika siku za mwisho. Ni mtazamo hasi wa
kutafsiri kinyume kwa kudai “Kanisa lilichukua nafasi ya Israeli”! Na
mpaka hivi sasa, kambi hii hailitambui taifa la Israeli lililopo hivi
sasa hapo Mashariki ya Kati!
Hata hivyo tukiyasoma maandiko ya
unabii wa Yesu Kristo kuhusu dhiki kuu inayotarajiwa kutokea hailitaji
kanisa na badala yake mlengwa mkuu ni Israeli:
“Bssi
mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli,
limesimama katika patakatifu (Asomaye na afahamu), ndipo walio katika
Uyahudi na wakimbilie milimani; naye aliye juu ya dari asishuke
kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; wala aliye shambani asirudi
nyuma kuichukua nguo yake. Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku
hizo! Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya
sabato.” (MT.24:15-20)
Maneno kama “Walio katika Uyahudi na
wakimbilie milimani..” na “ombeni kukimbia kwenu kusiwe siku ya Sabato”
yote yanadhihirisha kwamba tukio la chukizo la uharibifu litafanyikia
mjini Yerusalemu na wanaoagizwa kukimbilia milimani ni Wayahudi na sio
kanisa.
Makala haya ya kinabii yataendelea toleo lijalo. Kama
umesoma post hii nijulishe kwa ku-like na ukiweza wasambazie marafiki
zako. Nakusudia kujibu hoja zote pinzani kwa ushahidi wa maandiko na
tafsiri makini zisizo na utata ili “asomaye na afahamu”. Ubarikiwe sana.
Mwandishi; Askofu Sylivester Gamanywa
Unabii wa Yesu kuhusu hekalu la Yerusalemu-Sehemu 2 [Askofu Sylivester Gamanywa]
Share This
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment