Upendo hauhesabu kasoro - Kanisani Kwanza

Upendo hauhesabu kasoro

Share This
Inasikitisha.
Baada ya kumaliza kulinda amani na kupigana vita dhidi ya waasi huko mashariki ya kati, kijana ambae alikuwa ni mwanajeshi katika kikosi cha umoja wa mataifa aliamua kuwapigia simu wazazi wake.

"Baba na mama, ninarudi nyumbani, ila nina ombi moja kwenu. Ninae rafiki yangu nataka nije nae huko."
"Sawa njoo nae tu tutafurahi sana kumuona" wazazi wake walimjibu.
"Kuna kitu mnapaswa mjue wazazi wangu, huyu rafiki yangu aliumizwa vibaya na waasi baada ya kutekwa, amepoteza mkono wake wa kulia na mguu wa kushoto! Hana pa kwenda na ninataka nije nae tuishi wote pamoja hapo nyumbani."
"Poleni sana mwanangu, labda tukusaidie kupata sehemu nyingine ambako huyo rafiki yako ataishi, lakini sio hapa nyumbani."
"Hapana baba na mama mimi nataka aishi pamoja na sisi."

"Mwanangu mlemavu kama huyo atakuwa mzigo kwetu kumuhudumia."
"tunayo maisha yetu ya kuishi, na hatuwezi kukubali kitu kingine kiingilie haya maisha yetu ya furaha, ninafikiri wewe rudi tu nyumbani na usahau kuhusu huyo rafiki yako, atakuja kupata namna ya kuishi"


Kufikia hatua hii kijana alikata simu, wazazi hawakumsikia tena. Baada ya siku chache wazazi wake walipokea simu kutoka India, ilikuwa simu kutoka polisi katika mji wa New Delhi.
Wazazi waliambiwa kuwa Mtoto wao alikufa baada ya kuanguka kutoka juu ya jengo lenye ghorofa kumi, polisi walithibitisha pasina chembe ya mashaka kuwa kijana alijiua.
Wazazi walisafiri mpaka India, huko walienda katika mochwari ya jimbo kutambua mwili wa mtoto wao. Ni kweli alikuwa ni yeye, lakini kwa mshangao wakaona kitu ambacho hawakukitarajia kabisa! Kijana wao alikuwa na mkono mmoja na mguu mmoja.!


Wazazi wa kijana katika hadithi hii ni kama wengi wetu tulivyo. Tunaona ni rahisi zaidi kuwapenda wale wenye muonekano mzuri, ila hatupendi sana watu wenye kasoro mbalimbali mwilini. Tumewatenga na kuona kama hawana umuhimu wowote, kwamba maisha yao hayana thamani sawa na yako. Hii sio sawa kabisa. Onyesha upendo kwa wale wenye ulemavu, wapende na uwajali, dharau si jambo jema hata kidogo. Nakuombea kwa Mungu akupe moyo wa ujasiri wa kuwakubali watu jinsi walivyo, na akupe uelewa wa kuwatambua wale walio tofauti na wewe.


No comments:

Post a Comment